Ujuzi kwa Ajira katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara: Ajenda ya Dharura na ya Kipaumbele

Ujuzi kwa Ajira katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara: Ajenda ya Dharura na ya Kipaumbele Photo: Shutterstock

Zaidi ya kijana mmoja kati ya watano barani Afrika hayuko katika elimu wala hana ajira. Kampuni kubwa na za kati zinaendelea kubainisha kuwa nguvu kazi yenye ujuzi usiojitosheleza ni kikwazo katika uzalishaji. Ni sehemu ndogo tu ya watoto wanaoweza kusoma na kuelewa sentensi kwa urahisi wanapofikisha umri wa miaka kumi, uwezo ambao ni msingi muhimu na kiashiria cha mwelekeo wa ukuaji wa ujuzi kwa watoto. Katika kukabiliana na changamoto hizi za ujuzi, mwaka 2019 tulichapisha The Skills Balancing Act in Sub-Saharan Africa: Investing in Skills for Productivity, Inclusivity, and Adaptability. Katika ripoti hiyo, tuliangazia mizania miwili ambayo watunga sera wanapaswa kuizingatia wanapowekeza katika ujuzi. Kwanza, mvutano uliopo kati ya ujuzi unaochochea ongezeko la uzalishaji katika uchumi mzima na ujuzi unaokuza ujumuishaji wa makundi yaliyo hatarini zaidi. Pili, nchi zinapaswa kuweka mizania kati ya uwekezaji katika ujuzi msingi (ikiwemo ujuzi wa kiakili na wa kijamii-kihisia) na ujuzi wa kiufundi au ule mahususi kwa kazi fulani.

Katika makala hii, kila mmoja wetu — waandishi wakuu watatu — anatafakari suala muhimu ambalo tunaamini limekuwa na uzito mkubwa zaidi kuliko tulivyotarajia miaka saba iliyopita.

Indhira: Ushirikiano wa Kimataifa wa Ujuzi (Global Skills Partnerships) ni nyenzo ambayo haijatumika ipasavyo kuboresha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET). Ripoti yetu—na ripoti zilizotangulia pamoja na zilizofuata—ilibainisha uhusiano dhaifu kati ya mifumo ya TVET na waajiri kama changamoto kubwa kwa TVET barani Afrika, lakini haikuzingatia vya kutosha ushirikiano wa kimataifa kama suluhisho. Kwa kiasi kikubwa tulirejelea uhamaji katika muktadha wa wanafunzi kwenda kusoma nje ya nchi. Hata hivyo, ushirikiano wa moja kwa moja na waajiri, hasa kupitia ushirikiano wa kimataifa, unaweza kufanya TVET iwe na ulinganifu zaidi na mahitaji ya soko la ajira na kuboresha matokeo ya ajira ndani  na nje ya nchi. Ushirikiano huu wa Kimataifa wa Ujuzi unaziwezesha nchi za asili na nchi zinazopokea wahamiaji kuwekeza kwa pamoja katika mifumo ya elimu, kwa kuoanisha mafunzo na mahitaji ya sekta za uzalishaji pamoja na kuwezesha uhamaji wa wafanyakazi wenye ujuzi. Kanda ya Afrika iko katika nafasi nzuri zaidi kunufaika na mkabala huu kutokana na kuwa na idadi kubwa ya vijana katika dunia ambayo uchumi mwingi ulioendelea una idadi kubwa ya wazee. Kwa mfano, Ujerumani imeanzisha mradi wa majaribio wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ujuzi na Senegal pamoja na Ghana katika sekta ya ujenzi, ambao sasa unapanuliwa katika sekta kama nishati jadidifu na teknolojia ya habari, ukiwa na njia mbili za mafunzo zinazolenga ajira za ndani na ajira za nje ya nchi. Hivyo basi, ushirikiano wa kimataifa katika maendeleo ya ujuzi unaweza kupanua nguvu kazi zaidi ya mahitaji ya ndani na kuimarisha mifumo ya mafunzo kwa ushindani wa kimataifa.

David: Upatikanaji wa takwimu bora zaidi za ufuatiliaji wa wahitimu wa TVET ni jambo la dharura zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Vijana wanakabiliwa na machaguo mengi wanapotafuta mafunzo ya kuwawezesha kupata ajira. Nchini Ghana, kwa mfano, vijana wanaweza kuchagua mafunzo katika minyororo ya thamani kama korosho, usimamizi wa data za kompyuta, uchomeleaji vyuma, urembo, ufungaji wa mifumo ya umeme, na mengine mengi. Wanaweza pia kuchagua kati ya watoa mafunzo wa umma au binafsi. Je, kijana anawezaje kufanya uamuzi mzuri? Kuhakikisha kwamba taarifa kuhusu wastani wa mapato katika taaluma mbalimbali na programu za TVET zinapatikana kwa urahisi ni jambo muhimu ili kuwasaidia vijana kuelekea katika sekta zitakazowawezesha wao—na uchumi wao—kustawi. Baadhi ya nchi katika kanda kwa sasa zina tafiti za ufuatiliaji zinazofanyika mara kwa mara tu (kwa mfano Ghana au Afrika Kusini), lakini ni chache zilizo na mifumo ya kitaifa ya kutoa takwimu hizi. Mfumo wa Rwanda wa Kufuatilia Wahitimu (Graduate Tracking System) ni mfano mmoja. Ripoti yake ya mwaka 2024 inatoa maarifa si tu kuhusu ni programu zipi zilizopelekea viwango vya juu vya ajira—matengenezo ya barabara na upimaji wa vifaa vya ujenzi zote zilifanya vizuri—bali pia kuhusu muda ambao wahitimu walichukua kupata ajira. Ingawa kuna mapungufu, mpango huu ni hatua katika mwelekeo sahihi.

Nje ya kanda, Chile inatoa mfano mzuri, kwa kuwa na takwimu zinazohusu taaluma na taasisi mbalimbali—zikijumuisha TVET pamoja na elimu ya juu ya jumla—ili vijana waweze kufanya maamuzi yenye taarifa sahihi. Taarifa bora zaidi kuhusu faida za kiuchumi zinazotokana na elimu zinaweza kubadili maamuzi ya kielimu ambayo vijana hufanya kwa manufaa yao, na pia kutoa ishara muhimu kwa watoa mafunzo kuhusu namna wanavyopaswa kuboresha huduma zao.

Omar: Mwisho kabisa, mabadiliko ya teknolojia yanaongezeka kwa kasi isiyo ya kawaida. Miaka michache iliyopita, ripoti yetu kuhusu ujuzi ilisisitiza kuwa matarajio ya maendeleo ya kanda yalikuwa yakibadilishwa na mielekeo mikubwa ya kimfumo (megatrends), ikiwemo maendeleo ya haraka ya teknolojia za kidijitali na otomatiki, na ikaweka mkazo juu ya umuhimu wa kujenga uwezo wa kukabiliana na mabadiliko katika maisha yote ya kazi ya watu binafsi. Tulielezea “mizania ya ujuzi” kwa kuzingatia vipengele vitatu: utayari (readiness), yaani misingi ya ujuzi; fursa, yaani upatikanaji wenye usawa; na vichocheo, yaani mifumo na utawala, ili kuwawezesha watu kukabiliana na ulimwengu wa kazi unaobadilika kwa kasi. Kwa kutazama nyuma, ingawa tulitarajia kuwa mabadiliko endelevu ya teknolojia yangetikisa nafasi ya kihistoria ya sekta ya utengenezaji katika mabadiliko ya kimuundo ya uchumi, hatukutarajia kasi kubwa ambayo hasa ubunifu wa kidijitali—roboti na otomatiki, akili bandia, na majukwaa ya kidijitali—ungeenea duniani na kubadilisha mgawanyo wa kazi katika sekta mbalimbali ndani ya muda mfupi kiasi hicho. Uzoefu wa hivi karibuni wa Asia ya Mashariki unaonyesha kwa namna iliyo wazi fursa na hatari zinazolikabili bara la Afrika.

Kasi hii ya mabadiliko ya teknolojia ina athari za moja kwa moja kwa ajenda ya ujuzi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Bila kuwa na msingi imara katika ujuzi wa—kusoma na kuandika, kuhesabu, ujuzi wa kijamii-kihisia, na uelewa wa matumizi ya kidijitali—wafanyakazi na makampuni hupata ugumu wa kuzoea na kutumia kwa tija zana mpya za kidijitali. Mahitaji ya umahiri wa kidijitali yanaongezeka hata nje ya taaluma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), yakiwemo stadi za msingi na za kati za kidijitali zinazohitajika katika kazi za kila siku. Hili linaonesha umuhimu wa kujumuisha stadi za kidijitali katika programu za kuwajengea wafanyakazi ujuzi mpya (reskilling) na kuongeza ujuzi uliopo (upskilling), pamoja na kuhamasisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kutoa mafunzo ya ufundi stadi na elimu ya juu yanayoendana na mahitaji halisi ya soko. Pengo la matumizi ya teknolojia—hasa kwa wanawake—linapaswa kuzibwa kwa kuboresha miundombinu ya kidijitali, uunganishaji, uwezo wa kumudu gharama, umuhimu wa matumizi, na usalama mtandaoni, sambamba na mageuzi yatakayohakikisha mazingira wezeshi kwa makampuni kustawi na kuunda ajira zenye tija zaidi.

Katika mazingira ambayo teknolojia inaharakisha mabadiliko kwa kiwango kikubwa, vijana wasiokuwa na ujuzi unaohitajika wako katika hatari ya kuachwa nyuma katika fursa za siku zijazo. Huu ni wakati muhimu kwa watunga sera na washirika wao kuboresha upya fursa za maendeleo ya ujuzi kwa vijana katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Makala hii ni sehemu ya mfululizo wa kumbukizi unaoadhimisha miaka 15 ya mfululizo wa vitabu vya Africa Development Forum, vinavyochapishwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Agence Française de Développement.


Omar Arias

Deputy Chief Economist

David Evans

Director, Global Education and Child Well-Being Program, Center for Global Development

Indhira Santos

World Bank Lead Economist for People, Europe and Central Asia

Join the Conversation

The content of this field is kept private and will not be shown publicly
Remaining characters: 1000